MABAO YOTE YAFUTWA NA KOCHA MSIMBAZI

JUMA Mgunda, Kocha Mkuu wa Simba amesema kuwa matokeo yote ya mechi zilizopita amewaambia wachezaji wake wasahau na badala yake watazame kazi zinazofuata mbele.

Mgunda akishirikiana na Seleman Matola kashuhudia kikosi hicho kikishinda mechi tatu, sare moja na kuambulia maumivu kwenye mchezo mmoja kwenye ligi.

Ndani ya dakika 450, safu ya ushambuliaji imetupia mabao 10 huku ile ya ulinzi ikiokota mabao mawili kipa namba moja Aishi Manula kwenye mechi tatu hajatunguliwa.

 Mgunda amesema kuwa hakuna kitakachowasaidia ikiwa watakuwa wanakumbuka matokeo na mabao yaliyopita badala yake wanapaswa kufikiria kuanza upya.

“Tumeshinda mchezo wetu dhidi ya Mtibwa Sugar na kupata pointi tatu hilo limeisha ilikuwa hivyo hata tulipofungwa na Azam FC baada ya mchezo nilikaa na wachezaji na kuwaambia matokeo yaliyopita ni lazima tuyafute kichwani tuanze upya.

“Kila mchezo unapokwisha maana yake ni mwanzo wa maandalizi ya mchezo mpya hilo ni jambo la msingi, mazuri tunachukua na mabaya tunayachukua ili kuwa bora tukienda kwenye uwanja wa mazoezi na kufanya vizuri kwenye mechi,” amesema Mgunda.

Mechi tano za ligi kaongoza ilikuwa Tanzania Prisons 0-1 Simba, Simba 3-0 Dodoma Jiji, Yanga 1-1 Simba, Azam 1-0 Simba na Simba 5-0 Mtibwa Sugar