KOCHA MTIBWA AFICHUA UBORA WA SIMBA ULIPO

SALUM Mayanga, Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar amesema kuwa ubora wa Simba umejificha kwenye safu ya viungo jambo linalowafanya wacheze kwa kujiamini kila wanapokuwa na mpira.

Juzi, Simba iliibuka na ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Mkapa huku nyota wawili wa Mtibwa Sugar wakionyeshwa kadi nyekundu.

Mayanga amesema kuwa uimara wa Simba upo kwenye viungo makosa yao ilikuwa ni kukwama kuwazuia kwa umakini kutokana na kuelemewa na mzigo mzito.

“Tumefungwa mabao mengi inaumiza na hatukutaka iwe hivyo. Ukweli ni kwamba ubora wa Simba upo kwenye viungo hilo tulikuwa tunalitambua na tulifanyia kazi kubwa sehemu ya mazoezi kuwazuia.

“Kilichotokea kila mmoja ameona,wachezaji wetu wawili walionyeshwa kadi nyekundu, mpango kazi ulianza kuvurugika alipotoka Pascal Kitenge ikawa ni kazi kuwazuia viungo wa Simba na kadi ya pili ilipotolewa,(Cassian Ponera) tukalemewa kabisa kwenye mchezo wetu,” amesema Mayanga.

Kwenye mchezo huo safu ya viungo alikuwepo Clatous Chama, Mzamiru Yassin, Jonas Mkude, Augustino Okra na Pape Sakho.