>

WACHEZAJI YANGA WAMETOA AHADI HII KWA MABOSI

WACHEZAJI wa Yanga kwa pamoja wamewaahidi viongozi wa timu hiyo, kupambana kwa dakika 90 ili kuhakikisha wanarejresha imani ya mashabiki katika Kariakoo Dabi.

Dabi hiyo inatarajiwa kuzikutanisha Simba dhidi ya Yanga katika mchezo wa raundi ya kwanza ya Ligi Kuu Bara utakaochezwa Jumapili hii kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar.

Ni Jumatatu timu ilirejea kambini Kijiji cha Avic Town, Kigamboni nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam mara baada ya kutoka kutolewa na Al Hilal katika mchezo wa hatua ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

 Hersi amesema kuwa mara baada ya timu hiyo, kuingia kambini uongozi ulifanya kikao na wachezaji ambao walionekana kusikitishwa na kuumizwa na matokeo dhidi ya Al Hilal ambayo yamewakera mashabiki wa Yanga.

Hersi amesema kuwa katika kuelekea dabi, wachezaji wameahidi kupambana kufa au kupona ili kuhakikisha wanapata matokeo mazuri yatakayorudisha imani ya Wanayanga.

Aliongeza kuwa mara ya kikao hicho, wachezaji hao walihimizana kila mmoja kutimiza majukumu yake ya uwanjani pale atakapopata nafasi ya kuanza katika kikosi cha kwanza kitakachoanza kwenye dabi hiyo.

“Wachezaji wanajutia makosa yao waliyoyafanya ambayo yamesababisha kushindwa kufikia malengo ya kufuzu hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Afrika katika msmu huu.

“Hivyo wameahidi kurejesha imani ya mashabiki wa Yanga kwa kushinda katika dabi hii, ni baada ya kuondolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika kila mmoja ameahidi kuipambania timu katika mchezo huo.

“Tunafahamu haitakuwa rahisi, lakini wachezaji wenyewe upande wao wametoa ahadi hiyo kubwa ambayo ikifanikiwa, basi ninaamini mashabiki watarudisha imani kwa timu yao,” amesema Hersi.