SHIRIKA la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Watoto Duniani (Unicef) wameingia mkataba wa kufanya kazi na Klabu ya Yanga kwa muda wa miezi sita huku wakiahidi mengi mazuri.
Yanga wameingia mkataba huo hivi karibuni baada ya pande mbili kufikia makubaliano mazuri kati ya shirika hilo na klabu hiyo.
Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said amesema kuwa sababu kubwa ya kuingia mkataba na Unicef ambalo ni shirika la Umoja wa Mataifa ni kutokana na kuwa na mwendelezo mzuri wa kurejesha kwa jamii pamoja na hati safi, ni jukumu lao klabu kuunga mkono juhudi zitakazowezesha kushinda Uviko -19 na Ebola.
“Yanga na Umoja wa Mataifa kupitia Unicef tumeingia makubaliano ya kufanya nao kazi na kwa kuwa sisi ni klabu tunatoa huduma kwa jamii, maslahi ya kwanza ni kuhakikisha afya zao zinaimarika na kuwapa elimu kuhusu kupata chanjo ya Corona pamoja na kuwa na uelewa kuhusu ugonjwa wa Ebola.
“Gharama za mradi zinalipwa na Unicef na kuna ‘fee’ Yanga inalipwa, gharama zinategemea aina ya mradi ambao utafanyika. Kwenye miundombinu kikubwa ni fedha nguvu za wawekezaji zinatufanya kupata fedha Unicef wao ni watu makini na hii inatuongezea uaminifu na tutapata wawekezaji wakubwa zaidi,” amesema Hersi.
Kwa upande wa Fatimata Balandi, mwakilishi kutoka Unicef Tanzania amesema kuwa wanafurahi kufanya kazi na Yanga kwa ajili ya kuongeza nguvu kwenye mapambano dhidi ya Covid 19 na Ebola.
“Tunafurahi kufanya kazi na Yanga kwa ajili ya kuongeza nguvu kwenye mapambano dhidi ya janga la COVID 19 pamoja na Ebola ambapo tunaamini ndani ya miezi sita tutakuwa tumewafikia wengi na kuwafanya wawe na uelewa kuhusu Ebola na COVID 19,” amesema Fatimata.
Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Jackson Group, Kelvin Twisa alisema kuwa “Yanga inajihusisha zaidi na jamii yetu kuliko timu nyingine yoyote na UNICEF haibagui mshabiki wa timu yeyote ile.
“Yanga wanapotembelea jamii zetu huwa hawabagui mshabiki wa timu nyingine, maana hili sio swala la ushabiki ni swala la kijamii na Kitaifa kwa ujumla na kazi ya kuelemisha Jamii yetu tunayoenda kushirikiana na UNICEF tutahakikisha wapenzi wa mpira na Wananchi wote namna gani wanaweza kujikinga na maradhi haya,” amesema Twisa.