AZAM FC WANAZITAKA POINTI TATU ZA KMC

HASHEEM Ibwe, Ofisa Habari wa muda ndani ya Azam FC ameweka wazi kuwa wanawaheshimu wapinzani wao KMC lakini pointi zao tatu wanazitaka jambo linalowafanya wajiandae vizuri.

Ibwe amepewa majukumu kwa muda akichukua mikoba ya Zakaria Thabit ambaye amefungiwa kutojihusisha na masuala ya soka kwa muda wa miezi mitatu na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania, (TPLB) kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kuwashtumu waamuzi wa mchezo wa Tanzania Prisons 1-0 Azam FC.

Ibwe amesema kuwa wanatambua mechi ambazo zipo mbele yao ni ngumu ila wapo tayari kwa ajili ya kupata matokeo mazuri.

“Tunategemea kupata ushindi dhidi ya KMC, tumeshindwa kwenye Kombe la Shirikisho Afrika sasa tunategemea kuendeleza ushindi kwenye mechi za ligi pamoja na FA.

“Kwa wachezaji ambao watakosekana yupo Abdul Seleman, ‘Sopu’ yupo kwenye uangalizi maalumu kwa kuwa alipata maumivu hivi karibuni, wengine Daniel Amoah, Idd Suleiman,’Nado’, Ayoub Lyanga hawa wameshajiunga na timu,” amesema Ibwe.