BAADA ya kuondolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika Klabu ya Yanga inayonolewa na Kocha Mkuu, Nasreddine Nabi itashiriki Kombe la Shirikisho Afrika.
Leo Oktoba 18,2022 inatarajiwa kuchezwa droo kwa ajili ya mechi hizo za mtoano ambapo Yanga itakutana na mojawapo kati ya timu 16 ambazo zimeshinda hatua ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Yanga ina kibarua cha kucheza mechi ya mtoano kuwania kufuzu hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Shirikisho ikiwa ni namba mbili kwa ukubwa inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika, (CAF).
Mshindi wa jumla atacheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Miongoni mwa timu ambazo kuna uwezekano Yanga ikapangwa nao ni pamoja na RS Berkane, (Morocco), Gagnoa, (Ivory Coast) USM Alger, (Algeria), Real Bamako,(Mali), Pyramids, (Misri).
Ikumbukwe kwamba Yanga imetolewa kwa jumla ya mabao 2-1 dhidi ya Al Hilal ya Sudan.
Mchezo wao wa juzi ikiwa ugenini ilipoteza kwa kufungwa bao 1-0 na ule wa awali uliochezwa Uwanja wa Mkapa ililazimisha sare ya kufungana bao 1-1.
Miongoni mwa wachezaji ambao waliweza kuonyesha uwezo wao nchini Sudan ni pamoja na Khalid Aucho, Bernard Morrison na Fiston Mayele.
Jana kikosi cha Yanga kilirejea kutokea Sudan kwa ajili ya maandalizi ya mechi za kimataifa pamoja na ligi.
Mchezo ujao ni dhidi ya Simba ambao ni wa ligi unatarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa Oktoba 23.