BEKI WA KUPANDA NA KUSHUKA SIMBA KUIWAHI DABI

NYOTA wa Simba, Shomari Kapombe anatarajiwa kuwa miongoni mwa wachezaji ambao wataanza maandalizi kuelekea kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Yanga.

Simba na Yanga ambao ni watani wa jadi wanatarajiwa kumenyana Oktoba 23,2022 Uwanja wa Mkapa ikiwa ni mchezo wa Ligi Kuu Bara.

Mchezo huu unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kwa kuwa timu zote mbili mpaka sasa kwenye ligi hakuna ambayo imepoteza baada ya kucheza mechi tano.

Kapombe beki wa kupanda na kushuka hakuwa sehemu ya kikosi cha Simba kilichoshinda bao 1-0 na kutinga hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya de Agosto ya Angola.

Pia hakuwa sehemu ya kikosi kilichocheza mchezo wa awali ugenini na kushind kwa mabao 3-1 jambo lililoifanya Simba kutinga hatua ya makundi kwa jumla ya mabao 4-1.

Sababu kubwa ambayo imemfanya nyota huyo asiwe sehemu ya kikosi cha Simba ni majeraha ambayo yalikuwa yanamsumbua na kwa sasa anaendelea vizuri.

Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba amesema kila kitu kinakwenda sawa kuhusu mchezaji huyo.

“Maendeleo ya Kapombe anazidi kuimarika amekosekana kwenye mechi za hivi karibuni kwa sasa tayari ameanza mazoezi na kwa mechi zijazo baada ya kumalizana na de Agosto anaweza kuanza mazoezi na wachezaji wenzake na kuwa tayari kwa mujibu wa ripoti,” amesema.