>

SIMBA YAPEWA PONGEZI NA YANGA KIMATAIFA

KASI waliyoanza nayo Simba katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika imemuibua Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe ambaye amekubali mziki wa watani zao hao na kuwatakia kila la kheri katika safari yao ya kusaka tiketi ya kufuzu hatua ya makundi kupitia mchezo wao wa marudiano dhidi ya C.D de Agosto ya Angola.

Jumapili iliyopita Simba wakicheza ugenini kwenye Uwanja wa Novemba 11, nchini Angola walifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya kwanza.

Simba na Yanga zote Jumapili hii zinatarajia kushuka uwanjani katika michezo yao ya mkondo wa pili, ambapo Simba watakuwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, huku Yanga wao wakicheza kwenye Uwanja wa Al Hilal nchini Sudan.

Akizungumzia matokeo hayo ya Simba, Kamwe alisema: “Sisi kama Yanga tunawapongeza wenzetu kwa kwa ushindi wao, pia tunawatakia kila la kheri katika mchezo wao wa marudiano na hii sio kwa Simba pekee, bali kama taasisi tunawatakia kila la kheri Azam na Kipanga FC.

“Tunatamani kuona timu zote nne zinafuzu hatua ya makundi kwani kwa kufanya hivyo hii ina maana kuwa tutakuwa na nafasi nzuri ya kuongeza pointi za ushiriki wetu kimataifa.”