UMA Mgunda, Kocha Mkuu wa Simba ameweka wazi kuwa mafanikio ambayo yanapatikana ndani ya timu hiyo ni kutokana na benchi la ufundi makini pamoja na ushirikiano kutoka kwa viongozi na mashabiki.
Mgunda amekuwa na mwendo mzuri ndani ya Simba baada ya kupewa kibarua cha kuinoa timu hiyo ambapo mchezo wake wa kwanza ilikuwa dhidi ya Big Bullets ugenini na Simba ilishinda mabao 2-0 kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kocha huyo pia mchezo wake wa kwanza wa ligi ilikuwa dhidi ya Tanzania Prisons, Uwanja wa Sokoine, kikosi hicho kilishinda bao 1-0 na kusepa na pointi tatu muhimu.
Mgunda amesema:”Ni kweli wachezaji wamekuwa wakifanya kazi nzuri na matokeo yanapatikana jambo ambalo tunamshukuru Mungu kwa yote.
“Benchi la ufundi limekuwa likifanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na hasa Seleman Matola ambaye ni msaidizi huyu ni zaidi ya msaidizi kutokana na kuwa ni nguzo ya mafanikio kwenye ufundi.
“Yeye amekaa na timu kwa muda mrefu anawajua wachezaji pia nimefanya naye kazi kwenye timu ya taifa ya Tanzania hivyo ni moja ya watu muhimu kwenye kazi na anaifanya kazi inakuwa rahisi,”.
Simba kwa sasa ipo kwenye maandalizi kuelekea mchezo wa marudio wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya de Agosto ya Angola unaotarajiwa kuchezwa Jumapili, Uwanja wa Mkapa.
Mchezo uliochezwa ugenini Simba ilishinda mabao 3-1 hivyo ina kazi ya kulinda ushindi huo ili kutinga hatua ya makundi.