MPAGO mpya unasukwa na Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi kuelekea mchezo wa kimataifa dhidi ya Al Hilal unaotarajiwa kuchezwa ugenini wikendi hii.
Ni kwenye mapigo ya mipira iliyokufa ambayo wamekuwa wakiipata kwa kuwataka wapigaji kutulia huku wao wakipunguza makosa wakiwa karibu na eneo lao la hatari.
Bernard Morrison na Aziz KI wamekuwa wakipewa majukumu ya kupiga mipira hiyo ambapo kwenye mchezo dhidi ya Al Hilal, Uwanja wa Mkapa Morrison alipiga kona tatu na Aziz KI alipiga kona 6.
Nabi amesema kuwa kazi kubwa ambayo wanaifanyia kazi ni kupunguza makosa yaliyopita pamoja na kuimarisha safu ya viungo kwenye matumizi ya mipira hiyo.
“Wapinzani wetu Al Hilal sio wakuwabeza tunawaheshimu na tunajua kwamba ni wazuri kwenye matumizi ya mipira ile ya kutenga hapo lazima sisi tujiandae kutofanya makosa mengi.
“Tukipata nafasi za kutumia mipira ya kutenga ni muhimu kutumia vizuri kwa sababu kwenye mashindano ya kimataifa kuna ugumu wa kupata nafasi kama hizo na malengo yetu ni kufanya vizuri kwa kupata matokeo chanya,” amesema Nabi.
Kikosi cha Yanga kimeanza maandalizi yao kwa sasa kwa ajili ya mchezo huo wa marudio.