YANGA WAJA NA MBINU MPYA

BAADA ya ubao wa Uwanja wa Mkapa kusoma Yanga 1-1 Al Hilal mastaa wa Yanga wamerejea kambini na kuanza mazoezi kwa ajili ya mchezo wao wa marudio.

Mpango mpya kwa sasa ni kuwarejesha mastaa wote kwenye ubora wao na kufanyia kazi makosa ambayo walifanya mchezo uliopita Oktoba 8,2022.

Jumapili ya Oktoba 16,2022 mchezo huo unatarajiwa kuchezwa nchini Sudan ambapo mshindi wa jumla atafuzu hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika.

Saa 3:00 usiku mchezo huo ambao utakuwa na ushindani mkubwa unatarajiwa kuchezwa na tayari mikakati inapangwa kuelekea mchezo huo.

Miongoni mwa nyota ambao wameanza mazoezi ni pamoja na kiungo mshambuliaji Bernard Morrison, Dickson Ambundo, Heritier Makambo na Fiston Mayele.

Nasreddine Nabi, Kocha Mkuu wa Yanga amesema kuwa wapo tayari kwa ajili ya mchezo ujao na wana imani ya kupata ushindi.

“Kupata sare kwenye mchezo wa kwanza haina maana kwamba kazi imekwisha, bado tuna nafasi ya kufanya vizuri mchezo wetu ujao na kutimiza malengo.

“Hakuna ambaye anaamini kwamba mchezo utakuwa mwepesi hilo lipo wazi lakini tunafanya kila kitu kiwe sawa ili tupate ushindi,”.