MSAFARA wa wachezaji 24 wa kikosi cha Simba leo mapema Oktoba 8,2022 wamekwea pipa la kukodi kuelekea Angola.
Ni kwa ajili ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya de Agosto unaotarajiwa kuchezwa kesho, Oktoba 9, Uwanja wa Novemba 11 uliopo Angola.
Miongoni mwa wachezaji ambao wapo kwenye msafara huo ni kipa namba moja Aishi Manula, Beno Kakolanya na Ally Salim ambao wote hawa ni walinda milango.
Kwa washambuliaji ni watatu ambao ni Habib Kyombo, John Bocco ambaye pia ni nahodha pamoja na Moses Phiri. Miongoni mwa mabeki ambao wapo kwenye msafara huo ni Mohamed Hussein na Joash Onyango.
Juma Mgunda Kocha Mkuu wa Simba amesema wanatambua wapinzani wao uimara wao ulipo na udhaifu wao ulipo hivyo watapambana kupata matokeo.
“Tunatambua uimara wa wapinzani wetu ulipo na madhaifu yao yalipo, tutatumia madhaifu yao kupata matokeo kwenye mchezo wetu ambao tunajua kwamba utakuwa mgumu,”.