KIMATAIFA KAZI IFANYIKE KWELI NGOMA NI NZITO

IKIPIGWA sana ngoma mwisho inashindwa kuhimili mikikimikiki hiyo inagotea kwenye kupasuka jambo litakaloifanya iepukane na suala la kupigwa kwa mara nyingine.

Uzuri ni kwamba kwenye suala la upigaji na yule anayepiga lazima atambue kwamba itafika muda na yeye atapigwa tu kwani kuimba ni kupokezana.

Katika Ligi ya Mabingwa Afrika tunaona kwamba wawakilishi wetu kimataifa wanatamba kwamba watawapiga wapinzani wao kama ngoma.

Hakika hii ni imani kubwa ambayo inatakiwa kuwa kwenye mioyo ya wachezaji pamoja na mashabiki kuelekea kuishinda vita ya uwanjani.

Mashabiki wanapenda kuona timu inapata matokeo chanya na ile ngoma ya ushindi inapigwa kwa sauti kubwa ili kupata matokeo.

Wale ambao wanakwenda kushiriki kimataifa kama hawajafanya maandalizi mazuri basi kibao kinaweza kuwageukia na wao kama walipiga wengine kama ngoma nao watapigwa.

Hatupendi kuona wawakilishi wetu kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ambao ni Simba na Yanga na kwenye Kombe la Shirikisho ambao ni Azam FC wanakwenda kupigwa kama ngoma.

Pia wawakilishi pekee wa Zanzibar, Kipanga ambao wapo kwenye Kombe la Shirikisho nao wana kazi kubwa ya kufanya kupata ushindi dhidi ya Club Africain ya Tunisia.

Itapendeza ule mwendelezo wa Simba na Yanga kuwapiga wapinzani wao kuendelea kwa vitendo huku maneno yakiwa sehemu ya tambo kidogo.

Azam FC wao nao wana kazi kubwa ya kufanya kupata matokeo ugenini, wakati ni sasa kupeperusha bendera ya Tanzania kimataifa.

Hakika wawakilishi wetu mna kazi ya kufanya kwenye kusaka ushindi bila kujali mnapita kwenye hali gani ngumu.