Home Sports MTANZANIA IBRA CLASS, MMEXICO PINA KUMALIZA UBISHI LEO

MTANZANIA IBRA CLASS, MMEXICO PINA KUMALIZA UBISHI LEO

BONDIA Mtanzania Ibrahim Class anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa mpinzani wake kutoka Mexico, Gustavo Pina katika pambano la kimataifa la uzito wa feather litakalofanyika leo kwenye ukumbi wa Mlimani City.

Akizungumza mara baada ya kupima uzito jana, Pina alisema kuwa kamwe hawezi kupoteza mapambano mawili mfululizo na amekuja ili kurekebisha rekodi yake baada ya kupoteza pambano la ubingwa wa WBA dhidi ya bondia kutoka Panama, Anselmo Moreno mwezi Machi mwaka huu.

Alisema kuwa anajua anakabiliana na upinzani mkali kutoka kwa Class, lakini amejiandaa vilivyo kwani hawezi kurejea makosa yake tena.

Kwa mujibu wa rekodi, Class ameshinda mapambano 27 ambapo kati ya hayo, 12 kwa njia ya KO na kupoteza mapambano sita ambapo mawili kwa njia ya KO.

Pina ameshinda mapambano 10, matano kwa KO na kupoteza mawili yote kwa KO.

“Nimesafiri umbali mrefu kuja hapa Tanzania si kwa kushindwa, lengo kuu ni kushinda, hivyo Class ajiandae kwani siwezi kupoteza kamwe,” alisema Class.

Kwa upande wake, Class alisema kuwa pamoja na kuchukua tahadhari dhidi ya Pina, lengo lake ni ushindi na kuwaomba Watanzania kufika kwa wingi.

 “Ushindi wangu wa KO upo pale pale na si vinginevyo. Nimejiandaa vyema kwa ajili ya kuwapa heshima Watanzania na si  vinginevyo,” alisema Class.

Pambano hilo limeandaliwa na kampuni ya MO Boxing, ikiwa ni mara ya kwanza kwa kampuni hiyo chini ya mfanyabiashara maarufu, Mohammed Dewji.

Mratibu wa pambano hilo kutoka MO Promotion Ahmed Seddiqi alisema kuwa maandalizi yamekamilika na kutakuwa na mapambano sita ya utangulizi.

Pambano la kwanza la utangulizi litakuwa kati ya bondia nyota wa Ghana, Alfred Lamptey ambaye atapambana na bondia Abraham Ndauendapo kutoka Namibia huku Juma Choki akizichapa na bondia wa kutoka Mexico Jose Hernandez ambapo bondia kutoka Kenya Nicholas Mwangi atapimana ubavu na Emmanuel Mwakyembe wa Tanzania.

Pambano lingine litakuwa baina ya bondia Sameer Anwar dhidi ya Adam Mrisho huku Mwinyi Mzengela akizichapa na Sabari J na pambano lingine litakuwa baina ya Lulu Kayage dhidi ya Sadra Mohamed.

Mapambano hayo yamedhaminiwa na kampuni ya Azam TV, Boxer, MO XTRA, Mlimani City, KCB Bank, White Sands Resorts, Bajaj na OTAPP.

Previous articleAZAM FC KUIKABILI PRISONS, RUVU SHOOTING YAICHAPA COASTAL UNION
Next articleMERIDIANBET WAONGOZA ZOEZI LA USAFI UPANGA