KUMEKUCHA, MZUNGU SIMBA KUCHUKULIWA HATUA STAHIKI

UONGOZI wa Simba kupitia kwa Mtendaji Mkuu Barbara Gonzalez umeweka wazi kuwa straika wao Dejan Georgijevic hajafuata taratibu kwenye suala la kuvunja mkataba wake.

Nyota huyo maarufu kama Mzungu wa Simba, mapema jana Septemba 28,2022 kupitia ukurasa wake wa kijamii wa Instagram alibainisha kuwa amethibitisha mkataba wake wa ajira ndani ya Simba umesitishwa.

“Ninathibitisha kwamba mkataba wangu wa ajira umesitishwa kwa sababu za kukiukwa haki zangu za kimkataba na klabu. Asanteni sana mashabiki wa Simba kwa sapoti na upendo mlionipa,”.

Uongozi wa Simba umeweka wazi kuwa taarifa hizo wamezipokea kupitia mitandao ya kijamii jambo ambalo ni kinyume na utaratibu.

Taarifa hiyo imeeleza:”Uongozi wa Klabu ya Simba umepokea taarifa ya mchezaji Dejan Georgijevic ya kuvunja mkataba na klabu yetu.

“Hata hivyo tumesikitishwa na kitendo cha Dejan kuandika taarifa ya kuvunja mkataba kupitia mitandao ya kijamii bila kufanya mazungumzo na waajiri wake.

“Uongozi utachukua hatua stahiki juu ya mchezaji huyo kufuatia kuvunja mkataba bila kufuata utaratibu maalumu,”.