MZEE WA KUCHETUA KARUDI, KUWAKOSA SIMBA

KIUNGO wa Yanga, Bernard Morrison amezidi kuwa imara hali yake na tayari ameanza mazoezi na wachezaji wenzake.

Nyota huyo alipata maumivu kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam FC uliochezwa Uwanja wa Mkapa ambao waligawana pointi mojamoja.

Ubao wa Uwanja wa Mkapa ulisoma Yanga 2-2 Azam FC na Morrison aliyeyusha dakika 90 lakini alikuwa amepata maumivu.

Licha ya kuanza mazoezi nyota huyo hatacheza mechi tatu zinazofuata kwenye ligi za Yanga baada ya kufungiwa na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Bodi ya Ligi iliyo chini ya Shirikisho la Mpira Tanzania, (TFF).

Sababu ya nyota huyo mwenye bao moja ndani ya ligi ambalo aliwatungua Coastal Union Uwanja wa Sheikh Amri Abeid ni kile kilichoelezwa kuwa alimkanyanga kwa makusudi mchezaji wa Azam FC, Lusajo Mwaikenda.

Miongoni mwa mechi ambazo Morrison atazikosa msimu huu ni pamoja na ule dhidi ya Simba unaotarajiwa kuchezwa Oktoba 23, Uwanja wa Mkapa.

Pia atawakosa Namungo na Ruvu Shooting kwenye mtiririko wa adhabu hiyo na ametozwa faini ya milioni moja.