AZAM FC TATU ZAKE ZOTE UGENINI

KIKOSI cha matajiri wa Dar, Azam FC kina kete tatu ndani ya Septemba kwenye msako wa pointi tatu muhimu huku zote wakiwa ugenini kwenye dakika zote 270.

Timu hiyo ilianza kwa kutupa kete mbili ikiwa Uwanja wa Azam Complex iliambulia pointi nne kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Kagera Sugar na sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya Geita Gold.

Ipo chini ya Kaimu Kocha Daniel Cadena ambaye ni kocha wa makipa akichukua mikoba ya Abdi Hamid Moallin ambaye atapangiwa majukumu mengine ndani ya kikosi hicho.

Kete ya kwanza itatupwa dhidi ya Yanga, Septemba 6 Uwanja wa Mkapa kisha baada ya kupata kile watakachovuna wataibukia Mbeya, Uwanja wa Sokoine kusaka pointi sita kwenye mechi mbili.

Mchezo wao ujao itakuwa dhidi ya Mbeya City utakaochezwa Septemba 13 na ule wa pili utachezwa Septemba 30 itakuwa dhidi ya Tanzania Prisons.

Zakaria Thabit, Ofisa Habari wa Azam FC amesema kuwa kilakitu kinakwenda sawa na maandalizi yanaendelea.

“Maandalizi yanaendelea kwa kila mchezo na tunahitaji kufanya vizuri kwa kupata pointi tatu tunajua kwamba ushindani ni mkubwa,” amesema Thabit.