TAIFA STARS KAZI KUBWA IFANYIKE KUSAKA USHINDI

BADO kazi haijaisha kwa wachezaji wa Timu ya Taifa ya Tanzania, ‘Taifa Stars’ ambao leo wanatarajiwa kutupa kete ya pili kwenye mchezo wao wa pili dhidi ya Timu ya Taifa ya Uganda.

Dakika 90 za mwanzo zilikuwa na maumivu hasa baada ya Stars kuambulia kichapo cha bao 1-0 kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Mkapa.

Mchezo wa nyumbani matumaini yalikuwa makubwa kwa kila mmoja kuamini kwamba timu inaweza kushinda kuongeza nguvu kwenye tiketi ya kuwania kufuzu CHAN.

Haikuwa hivyo na mwisho kila mmoja alitoka akiwa na lake moyoni kutokana na Stars kupoteza wakiwa nyumbani katika dakika za lala salama.

Ipo hivyo mchezo wa mpira ni makosa pale ambapo Stars walifanya makosa wapinzani wao Uganda walitumia kuwaadhibu na sasa wanakwenda kwenye mchezo mwingine ambao wana nafasi ya kushinda.

Haitakuwa kwa wepesi ukizingatia benchi la ufundi ni jipya baada ya Kim Poulsen kuondolewa na presha kwa kila mmoja inaonekana kuwa juu.

Inawezekana kuna kitu kitaonekana kwa wachezaji leo lakini kinachotakiwa ni kila mmoja kujituma bila kuogopa kwenye mchezo wa leo.

Watanzania Stars ni yetu na kila mmoja anajukumu la kuongeza kuomba dua ili matokeo yawe chanya watakaporejea tukawapokee mashujaa wetu wakiwa na jambo la tofauti wametuletea.

Itakuwa hivyo wachezaji wakijituma na kuamini kwamba kama wao waliweza kushinda wakiwa ugenini basi dakika 90 zitakuwa zao wakiwa ugenini pia.