NABI:HAITAKUWA KAZI RAHISI KUTWAA UBINGWA

NASREDDINE Nabi, Kocha Mkuu wa Yanga ameweka wazi kuwa ushindani kwenye ligi ni mkubwa jambo ambalo linawafanya wazidi kujipanga kwa mechi zao.

Yanga ni mabingwa watetezi wa taji la ligi ambalo walitwaa msimu wa 2021/22 kutoka mikononi mwa watani zao wa jadi Simba.

Timu hiyo imecheza mechi mbili na kukusanya pointi sita, ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Polisi Tanzania na ilishinda mabao 2-0 dhidi ya Coastal Union.

Nabi amesema:”Msimu umeanza kwa upekee na kila timu inahitaji kupata matokeo chanya hili ni jambo la muhimu na zuri kwetu kwa kuwa linatufanya tuzidi kuwa imara.

“Haitakuwa kazi nyepesi kutetea ubingwa msimu huu kutokana na kila timu kujipanga lakini wachezaji wapo tayari kuona tunapata ushindi kwenye mechi zetu,” amesema.

Mchezo ujao Yanga inatarajia kucheza na Azam FC Uwanja wa Mkapa.

Azam FC wamekusanya pointi 4 kwenye mechi mbili ambazo wamecheza, ni ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Kagera Sugar na sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya Kagera Sugar.

Yanga mechi zote mbili ilicheza Uwanja wa Sheikh Amri Abeid ikiwa ugenini na Azam FC mechi zake zote ilicheza Uwanja wa Azam Complex ikiwa nyumbani.