KOCHA Mkuu wa Simba, Mserbia, Zoran Maki, amebadili uamuzi na haraka amembakisha kiungo wake mkabaji, Mnigeria, Victor Akpan kwa ajili ya kuendelea kuicheza timu hiyo.
Hiyo ikiwa ni siku moja tangu kocha huyo achukue uamuzi wa kuwaacha nyota wake watatu ambao John Bocco, Nassoro Kapama na Akpan.
Akpan ni kati ya wachezaji ambao awali waliondolewa katika mipango ya kocha huyo akikosa michezo mitatu ya mashindano, Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga na ile ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Geita Gold na Kagera Sugar.
Taarifa ambazo imezipata Spoti Xtra, juzi Jumanne jioni ndiyo Zoran alibadili mpango huo wa kumuacha Mnigeria huyo mara baada ya kikao kilichowakutanisha Bodi ya Wakurugenzi wa timu hiyo na kocha.
Mtoa taarifa huyo alisema hadi wanafikia makubaliano ya kumbakisha kiungo huyo, majadiliano makubwa yalikuwepo kati ya uongozi na kocha huyo ambaye kwa moyo mmoja amekubali aendelea naye.
Aliongeza kuwa, mara baada ya kufikia muafaka huo, kiungo huyo akapewa taarifa za kuingia kambini jana Jumatano jioni tayari kwa ajili ya kuendelea na maandalizi ya michezo ijayo ikiwemo ya kirafiki ambapo Simba imealikwa Sudan.
“Akpan haendi popote na badala yake ataendelea kuichezea Simba kwa msimu huu, hiyo ni baada ya majadiliano ya muda mrefu kati ya kocha na uongozi wa timu uliokaa jana (juzi) Jumanne jioni.
“Muafaka umekuja baada ya kocha kukubali kumuangalia Akpan kwa kumpa nafasi ya kucheza katika michezo ya ligi na kimataifa.
“Leo (jana) Jumatano atakuwepo katika orodha ya wachezaji watakaoingia kambini kujiandaa na michezo ijayo ya ligi na kimataifa,” alisema mtoa taarifa huyo.
Akizungumzia hilo, Akpan alisema: “Mimi sina taarifa za kutaka kuachwa, kwangu naona ni kama tetesi tu.
“Leo (jana) Jumatano nitaingia kambini pamoja na wachezaji wenzangu wote kujiandaa na michezo ijayo ya ligi na michuano ya kimataifa, hivyo sitakwenda popote, nitabaki hapa Simba.”