WACHEZAJI NI MUDA WA KULINDANA WENYEWE

KUCHANGAMKA kwa mzunguko wa kwanza na wa pili kwenye ligi kumetokana na maandalizi mazuri ambayo yalifanywa na timu husika hilo halipingiki.

Kwa timu ambazo zilikwama kupata matokeo hapo kuna sehemu ya kuangalia namna ya kuweza kuboresha na kuwa bora wakati ujao.

Katika mechi za mzunguko wa kwanza na wa pili inaonekana kwamba wachezaji wanatumia nguvu kubwa kusaka ushindi.

Pia wapo wachezaji ambao wanapata maumivu kutokana na kuchezewa faulo kwenye uwanja jambo ambalo linapaswa lisipewe nafasi wakati ujao kwenye mzunguko wa tatu mpaka wa mwisho.

Ukweli ni kwamba maisha ya mchezaji yanategemea mpira na ikitokea akapata maumivu akawa nje ya timu kwa muda ni sababu ya yeye kushindwa kutengeneza ugali wake.

Familia inamtegemea kijana ambaye anacheza mpira hivyo kuanzia wachezaji kuna umuhimu wa kujali afya ya mwingine kabla ya kumchezea faulo.

Wapo wachezaji ambao hawatakuwa kwenye majukumu ya timu zao kwenye mzunguko wa tatu inatokana na kutokuwa fiti na wengine waliumizwa na wachezaji uwanjani kwenye mapambano ya kusaka pointi tatu.

Wapo wengine ambao walipata maumivu hayo wakiwa kwenye mazoezi na kufanya mambo kwao kubadilika hivyo kwa muda uliopo kwa sasa ni muhimu kuwa makini.

Kila mmoja anakazi ngumu kufanya kazi ya kusaka ushindi na kinachotakiwa ni umakini katika kutimiza majukumu.

Hakuna haja ya kutumia nguvu kubwa kwenye mazingira ambayo hauwezi upata mpira inabidi ukubali yaishe.