KOCHA NABI AMTABIRIA MAKUBWA MAKI

NASREDDINE Nabi,Kocha Mkuu wa Yanga amesema kuwa Zoran Maki kocha wa Simba anapaswa apewe muda kuiunda timu ya ushindani kwa kuwa bado kila kitu kwake ni kipya.

Maki alikabidhiwa mikoba ya Pablo Franco ambaye alichimbishwa Mei 31, 2021 baada ya kuvuliwa taji la Ngao ya Jamii kwa kufungwa bao 1-0 dhidi ya Yanga katika hatua ya nusu fainali.

Nabi amesema kuwa anatambua uzoefu wa Maki na kwa timu ambazo kazifundisha aliweza kufanya kazi kubwa.

“Natambua uzoefu wa kocha wa Simba,(Maki) hata timu ambazo amefundisha ni kubwa Afrika na alifanya vizuri kwa kuwa yupo hapo inabidi apewe muda aweze kuunda kikosi chake na kupata uzoefu.

“Ukitazama namna kikosi cha Simba kilivyo kuna wachezaji wengi wapya na wageni nao wanahitaji muda ili waoneshe kile ambacho wanacho hivyo nina amini kwa msimu ujao kwenye ligi kutakuwa na kitu cha kipekee kwa kila timu,” amesema Nabi.

Taji la kwanza kwa msimu wa 2022/23 ambalo ni la Ngao ya Jamii lipo mikononi mwa Yanga ikilitetea kwa mara nyingine baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Simba.

Mchezo wa kwanza wa ligi, Maki ameweza kushuhudia timu hiyo ikishinda mabao 3-0 dhidi ya Geita Gold.