ZORAN Maki,Kocha Mkuu wa Simba amesema kuwa watajitahidi kushinda kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga.
Leo Agosti 13, Simba inatarajia kumenyana na Yanga kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa.
Maki amesema kuwa anawaheshimu wapinzani wao Yanga lakini watafanya kila namna kwenye kusaka ushindi watakapokutana.
“Tunakutana na timu ambayo inawachezaji wazuri na ninajua kwamba unakuwa ni mchezo wa ufunguzi huo ni muhimu kuanza kwa ushindi hivyo tutajitahidi kushinda mbele ya Yanga kwenye mchezo wa dabi.
“Ipo wazi kwamba kila nchi kuna dabi na maandalizi yake pamoja na namna ya kuweza kucheza huwa inakuwa tofauti lakini nina amini wachezaji ambao tupo nao wapo tayari kuendeleza ushindani,” amesema Maki.
Ni kipa namba moja Aishi Manula anatarajiwa kukosekana kwenye mchezo wa leo kwa kuwa bado hajawa fiti hivyo langoni anaweza kuanza Beno Kakolanya.
Kuelekea kwenye mchezo wa leo,Agosti 12 rais wa heshima, wa Klabu ya Simba Mohammed Dewji alikutana na kuongea na wachezaji kuelekea mchezo wa Ngao ya Jamii ambao ulihudhuriwa na viongozi wengine wa Simba ikiwa ni pamoja na Mtendaji Mkuu, Barbra Gonzalez.