MASHINE mbili za kazi ndani ya kikosi cha Yanga ni uhakika kuwa ndani ya kikosi hicho baada ya kuongeza madili mapya mpaka 2024.
Ni Djuma Shaban mzee wa kumwaga maji na mchezaji bora wa msimu wa 2021/22 Yannick Bangala wote wawili raia wa DR Congo wameongeza kandarasi ya miaka miwili.
Wawili hao walihusika kwenye mabao 9 kati 49 yaliyofungwa na timu hiyo iliyomaliza msimu ikiwa nafasi ya kwanza na pointi 74 kibindoni.
Djuma alicheza mechi 24 na aliyeyusha dk 2,085 alifunga mabao matatu na alitoa pasi tano za mabao kwa upande wa Bangala yeye alicheza mechi 23 alitoa pasi moja ya bao na aliyeyusha dk 2,074.
Cedric Kaze,Kocha Msaidizi wa Yanga amesema kuwa wachezaji wote walifanya kazi kubwa msimu uliopita kulingana na tathimini yao.
“Tulifanya tathimini ya kila mchezaji na timu kiujumla na ukweli ni kwamba kila mchezaji alifanya vizuri na hilo linatokana na matokeo ambayo tumeyapata,” alisema Kaze.