HANS PLUIJM KUTAMBULISHWA SINGIDA BIG STARS

INAELEZWA kuwa Kocha Mkuu wa Singida Big Stars,Hans Pluijm atatangazwa rasmi na benchi lake jipya Uwanja wa Liti Agosti 4 siku ya tamasha lililopewa jina la Big Day

Habari zinaeleza kuwa Singida Big Stars imefikia hatua nzuri na Pluijm kuweza kurejea kwa mara nyingine tena kwenye ardhi ya Tanzania aliwahi kuifundisha Yanga,Azam FC na Singida United.

Singida Big Stars inatarajiwa kuleta ushindani mkubwa msimu ujao baada ya kupanda Ligi Kuu Bara kutoka Championship mbapo ilikuwa inaitwa DTB.

Agosti 2 Singida Big Stars iliweza kutangaza mdhamini wao mkuu ambaye ni SportPesa huku wakiweka wazi kuwa ni dili nono na lenye faida kwao.

Ofisa Habari wa Singida Big Stars,Hussein Masanza amesema kuwa kumekuwa na orodha ndefu kuhusu benchi la ufundi ila wakati ukifika kila kitu kitakuwa wazi.

“Walianza kusema Zahera,(Mwinyi) na sasa ni Pluijim naona orodha inazidi kuwa ndefu hivyo ni suala la kusubiri na kuona kwani wakati unakuja.

“Agosti 4 tutatambulisha benchi la ufundi na orodha ya wachezaji wote wa kikosi kupitia event,(tukio) yetu ya Big Day mkoani Singida,” alisema Massanza.

Siku hiyo Singida Big Stars itatambulisha pia uzi mpya na itacheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Klabu ya Zanaco.