KAMPUNI ya Michezo ya kubashiri ya SportPesa imeingia mkataba wa makubaliano wenye thamani ya Shilingi Bilioni 12.33 na Yanga SC kwa kipindi cha miaka mitatu, baada ya mkataba wa awali wa miaka mitano kufika ukingoni.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya SportPesa, Abbas Tarimba amesema mkataba huo utakuwa wa miaka mitatu wenye thamani ya kiasi hicho cha fedha huku Klabu hiyo ikitarajiwa kupata Shilingi Bilioni 4 kila mwaka.
“Tumeingia mkataba huu na Yanga SC ambao umepanda thamani kubwa, tofauti na mkataba uliopita, walikuwa wanapata Bilioni 1 kwa mwaka, sasa hivi tumeongeza thamani kwa kuwapa Shilingi Bilioni 4 kwa kila mwaka kwenye sehemu ya mkataba wetu.
“Yanga SC ikishinda ubingwa wa ligi msimu ujao watapata bonasi ya Shilingi Milioni 150 tofauti na zamani walikuwa wanapata Shilingi Milioni 100, lakini kwenye Michuano ya ASFC wakifika Fainali watapata bonasi ya Shilingi Milioni 75 na wakishinda Ubingwa wa Michuano hiyo watapata Milioni 112”, ameeleza Tarimba.
Kwa upande wake, Rais wa Klabu hiyo, Mhandisi Hersi Said ameshukuru Uongozi wa Kampuni hiyo ya SportPesa kwa kuingia makubaliano ya mkataba huo na Klabu ya Yanga inatarajia kufanya vizuri msimu ujao kutokana na hamasa hiyo sanjari na usajili uliofanywa kuelekea msimu ujao wa mashindano.
“Haikuwa rahisi kufika makubaliano haya ambayo leo, sisi na SportPesa tunasaini makubaliano haya, tunaamini kazi kubwa imefanywa na Uongozi wa Yanga SC chini ya Dkt. Mshindo Msolla ambaye ni Mwenyekiti Mstaafu na Wajumbe wengine wa Kamati ya Utendaji.
“Mafanikio haya ya Uongozi uliopita kwa kiasi kikubwa yamesababisha Yanga SC kutwaa mataji matatu ya Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Soka Tanzania Bara na Michuano ya Kombe la Shirikisho (ASFC) msimu wa 2021-2022, tunaamini msimu ujao tutafanya makubwa zaidi kwa Uongozi wa sasa uliopo madarakani,” amesema Hersi.
Ilikuwa ni Julai 27 na sasa Yanga wapo kwenye maandalizi ya Wiki ya Mwananchi inayotarajiwa kufika kileleni Agosti 6 na kauli mbiu ni Byuti Byuti.