JUMLA ya timu saba za Maveterans zitashiriki katika bonanza maalum la mpira wa miguu litakalofanyika leo Jumapili (Julai 31, 2022) kwenye Uwanja wa Bora Kijitonyama.
Bonanza hilo limeandaliwa na taasisi ya ukaguzi wa mahesabu, ushauri wa kifedha, biashara na masuala ya kodi ya Techno Auditors kwa kushirikiana na timu ya Kijitonyama Veterans.
Mkurugenzi Mtendaji wa Techno Auditors, Lupiana Michael amesema kuwa mbali ya kuhamasisha maendeleo ya michezo, bonanza hilo litakuwa maalumu la kuadhimisha au kusheherekea miaka 10 tangu kuanzishwa kwa taasisi yao.
Lupiana alizitaja timu hizo kuwa ni Tanga Veterans, Tabora Veterans, Goba Veterans, Uganda Veterans, Kijitonyama Veterans, Posta Veterans and Techno Auditors veterans.
“Tumeweka masharti kwa timu zote shiriki ili kuwa na bonanza lenye mafanikio ya hali ya juu.Kwa mfano wachezaji vijana watakao ruhusiwa ni wanne (4). Kipa anaweza kuwa kijana pia na hatozuiliwa kucheza. Timu inaruhusiwa kuwa na vijana wengi, ila watakaoruhusiwa ni hao wanne tu.
“Kanuni hiyo ina maanisha kuwa hata wakati wa ubadilishaji wa wachezaji lazima idadi ya vijana izingatiwe kwani akitoka kijana, ataingia kijana na haiwezekani atoke mzee aingie kijana. Lengo ni kuwapa nafasi wachezaji wenye umri zaidi ya miaka 35 kupata muda wa kucheza,” amesema Lupiana.