WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa alikuwa mgeni rasmi katika toleo la tatu la NBC Dodoma Marathon.
Ilikuwa ni Marathon iliyokuwa na ushindani mkubwa na ilivutia zaidi ya washiriki 4,000 kutoka nchi 8 tofautitofauti ambayo walishiriki.
Lengo kuu ni kutafuta fedha za kusaidia mapambano dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi nchini Tanzania kupitia Taasisi ya Saratani ya Ocean Road.
Zaidi ya milioni 200 zilikusanywa kusaidia wanawake wenye saratani ya mlango wa kizazi.Katika miaka miwili iliyopita, zaidi ya milioni 300 walikusanya na kuwezesha uchunguzi wa wanawake zaidi ya 9,000; 550 waligunduliwa na saratani na kwa sasa wanaendelea na matibabu.
Majaliwa ameipongeza Benki ya NBC kwa kuandaa Marathoni ya kuchangisha fedha, kupitia “NBC Dodoma Marathoni,” kwa lengo la kusaidia mapambano dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi nchini Tanzania.
Akizungumza katika mbio za marathoni mjini Dodoma, Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa Serikali inathamini jitihada za sekta binafsi za kuungana mkono katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazoikabili jamii.
“Serikali inatambua kazi nzuri ya mchango wa kijamii uliofanywa na Benki ya NBC kwa miaka mingi. Tunashukuru kwa ubunifu wa kushirikiana na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road na Chama cha Riadha Tanzania kuendeleza mbio hizi za marathoni zinazolenga kukusanya fedha za kusaidia mapambano dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi nchini Tanzania.
“Saratani ya shingo ya kizazi, ingawa inaongoza kwa kupoteza maisha ya wanawake nchini Tanzania, inaweza kuepukika na kutibika iwapo itagundulika mapema. Serikali inaunga mkono juhudi zote za kuongeza ufahamu wa wanawake na kuokoa maisha yao ya thamani,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi amesema benki hiyo inafuraha kuandaa kipindi kingine cha mbio za NBC Bank Dodoma Marathon baada ya mafanikio.
“Baada ya matoleo mawili yenye mafanikio ya mbio za Marathon hapa Dodoma, tunayo furaha kuandaa toleo la tatu. Pesa zote zilizopatikana, karibu TZS200 milioni, zitaelekezwa katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road kusaidia mapambano ya wanawake dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi.
“Ninayofuraha kutangaza kwamba katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, mbio za Marathoni zilikusanya zaidi ya TZS300 milioni, ambazo zilisaidia kupima wanawake zaidi ya 9,000 wanawake, 550 kati yao waligundulika kuwa na saratani na kwa sasa wanaendelea na matibabu.
“Nashukuru kwa uungwaji mkono wote kutoka pembe zote za bara hili, huku watu wakijumuika nasi katika kazi hii adhimu. Benki ya NBC ina bahati ya kuweza kukusanya fedha ili kuokoa maisha na kuleta matumaini kwa familia,” amesema.