HATIMAYE mshambuliaji wa Yanga, Fiston Mayele amevunja ukimya juu ya mkataba wake na Yanga, ambapo ameweka wazi kuwa yeye si mchezaji wa mkopo bali alisaini mkataba wa miaka miwili na bado amebakiza mwaka mmoja.
Mayele alijiunga na Yanga Agosti 1, 2021 kwa mkataba wa miaka miwili akitokea katika Klabu ya AS Vita ya kwao DR Congo, hivyo mkataba wake unatarajiwa kuisha mwishoni mwa msimu ujao.
Akizungumza mara baada ya kuwasili katika kambi ya Yanga, Mayele ametumia fursa ya kurejea kwake kuwaeleza mashabiki kuwa, bado yupo Yanga hadi mwisho wa msimu ujao, ila ni kweli alikuwa na ofa nyingi ikiwemo ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, Raja Casablanca ya Morocco na Al Hilal ya Sudan, lakini amekataa ofa zote hizo ili aichezee Yanga.
“Mimi sipo Yanga kwa mkopo ila nilisaini mkataba wa miaka miwili na kwamba, mkataba wangu utaisha mwishoni mwa msimu ujao, kuhusu tetesi zilizokuwa zikiendelea ni kweli kwamba, nilipata ofa nyingi sana ikiwemo ile ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, ila mbali na ofa hiyo pia nilipata ofa kubwa sana kutoka Raja Casablanca ya Morocco.
“Kiukweli nimeshindwa kusema niachane na Yanga, hivyo uamuzi wangu ni kuutumikia mkataba wangu mpaka mwisho, maana nilisaini miaka miwili na tayari mmoja umeshakatika, hivyo mambo yote yaliyokuwa yakisemwa kwa sasa naomba ieleweke wazi kuwa mimi ni mchezaji halali wa Yanga,” amesema Mayele.