MUDA uliobaki kwa sasa ni wa dhahabu kwa timu zote ambazo zinajiandaa na msimu ujao wa 2022/23 ambao unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.
Kwa sasa siku zinahesabiki hasa kuelekea mwanzo wa msimu ujao ukizingatia kwamba Agosti 13 mchezo wa Ngao ya Jamii unatarajiwa kuchezwa.
Huu mchezo ni maalumu kwa ajili ya ufunguzi wa ligi na ina maana kwamba pazia linafunguliwa kwa ajili ya kuanza msimu mpya.
Kuna timu bado zinajipambanua kwamba zipo sokoni zinasaka wachezaji,huu muda unatosha kukamilisha hesabu hizo na kama bado maongezi ni magumu kwa hao wachezaji basi muhimu kuwa na mpango wa pili.
Ikiwa mchezaji atakuja kupatikana wakati tayari timu imeshamaliza maandalizi ya msimu mpya ina maana kwamba mchezaji atakuwa mgeni mara mbili kwenye kikosi.
Hakuna namna nzuri ya kuwa hivyo kwa wachezaji kupambana mara mbili kutafuta nafasi ya kuwa kikosi cha kwanza kwa sababu ya kuchelewa kuingia kambini.
Muhimu kwa timu ambazo hazijakamilisha usajili kuweza kufanya usajili mapema na kutumia muda huu wa dhahahabu kuweza kupata wachezaji ili waweze kujiunga na timu kambini.
Kwa wale ambao wapo kambini iwe ni kambi kwelikweli maana msimu ukianza mashabiki wao wanahitaji matokeo ya furaha ambayo ni ushindi.
Wale ambao wamepata changamoto mpya wana kazi ya kutumia muda wa dhahabu kufanya kweli ili wapenye kikosi cha kwanza.