SPORTPESA WAISHUKURU SIMBA,WAJIVUNIA MAFANIKIO

MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi wa SportPesa, Tarimba Abbas, amewatakia heri Klabu ya Simba kwa kuingia mkataba mpya na M-Bet, huku akiwashukuru kwa ushirikiano wao ndani ya miaka mitano ya udhamini wao.

 Tarimba amesema ulikuwa mkataba wa mafanikio makubwa, hivyo baada ya kupata barua yao ya kuachana nao rasmi walifurahi maana wana mengi ya kujivunia kutoka kwao ikiwa ni pamoja na mafanikio waliyofikia Simba katika soka.

SportPesa amekuwa mdhamini wa vilabu vyote viwili vikubwa nchini Tanzania vya Simba na Yanga, kitendo cha Simba kusaini mkataba mpya na M- Bet ni ishara tosha kuwa SportPesa anaweza kubaki kuwa mdhamini wa Klabu ya Yanga kama atafanikiwa kusaini mkataba mpya na mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya NBC.

Tarimba ameweka wazi kuwa walipokea barua ya Simba kusitisha mkataba na SportPesa mara baada ya msimu kumalizika.

“Labda watu hawafahamu kuwa sisi SportPesa ndio tulikuwa wa kwanza kuingia katika udhamini kwenye soka,tukiingia katika udhamini huo tulikuta makampuni zaidi ya matano yapo nje ya udhamini.

“Katika kipindi hicho chote cha udhamini kuaniza 2017/2022 tumefanikisha mengi ndani ya Simba ikimwemo robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa misimu miwili pia kuchukua Kombe la Ligi na Shirikisho.

“Pia wachezaji wengi wa kigeni wamekuwa kimbilio lao Simba kwa kuja kucheza kipindi hicho havikuwepo vitu kama hivi, tunajivunia SportPesa kwa kuifanya Simba bora na imara,”.