FELIX Minziro, Kocha Mkuu wa Geita Gold ameweka wazi kuwa kasi ya vijana wake kimataifa na kwenye ligi kwa msimu ujao wa 2022/23 itakuwa ni moto wa kuotea mbali.
Geita Gold msimu ujao itashiriki michuano ya kimataifa katika Kombe la Shirikisho baada ya kumaliza ligi ikiwa nafasi ya nne kwenye msimamo na pointi 46.
Minziro amesema kuwa kwa mwendo ambao walimaliza ligi msimu huu anaamini watakuja kwa mwendo wa kipekee hasa msimu ujao.
“Ikiwa nitaendelea kuwa ndani ya Geita Gold wakati ujao kwa msimu mpya itakuwa ni moto wa kuotea mbali hasa kwa vijana wangu ambao wanapenda kufundishika na wanapenda kazi yao.
“Inabidi ukumbuke kwamba hapo ni mimi nitaanza na timu mwanzo kabisa kwani msimu huu nilianza baada ya mechi 4 kupita unadhani nini kitatokea? Tutafanya makubwa zaidi,” amesema Minziro.
Minziro alikuwa kwenye orodha ya makocha wanaowania tuzo ya kocha bora pamoja na Juma Mgunda wa Coastal Union ambao ni wazawa na tuzo ilikwenda kwa Nasreddine Nabi wa Yanga.