MSHAMBULIAJI mpya wa Simba, Moses Phiri, amesema kuwa anategemea kupata ushirikiano mzuri ndani ya Simba kutoka kwa kiungo Clatous Chama na kuifanya timu hiyo kuwa tishio zaidi kwa msimu ujao jambo ambalo anaamini litaisaidia kurejea katika makali yake.
Phiri ndio usajili wa kwanza kutambulishwa ndani ya Simba kwa msimu huu ambapo mchezaji huyo ana uraia wa Zambia kama ambavyo ipo kwa Chama ambaye pia ni raia wa Zambia.
Phiri amesema kuwa anaamini kwa msimu ujao atapata usharikiano mzuri kutoka kwa Chama jambo ambalo litakuwa faida kwa Simba katika kuhakikisha kuwa wanairejesha Simba katika ubora wake.
“Nategemea kupata ushirikiano mzuri kutoka kwa Chama kuelekea msimu ujao, Chama tumecheza wote katika timu ya taifa ya Zambia, namfahamu vyema, ni mchezaji mzuri sana na naamini kwa pamoja tutaipa ubora Simba kwa msimu ujao.
“Simba msimu huu nafahamu haijakuwa katika ubora wake lakini naamini kwa msimu ujao kila kitu kitakuwa sawa, tutajitoa kwa uwezo wetu wote tushinde mataji,” amesema mchezaji huyo.