ILALA FC MABINGWA LIGI YA SOKA LA UFUKWENI

MABINGWA wa Ligi ya Soka la Ufukweni msimu wa 2021/22 ni Ilala FC baada ya ushindi kwa penalti 4-3 dhidi Mburahati FC kwenye mchezo uliochezwa jana, Viwanja vya Coco Beach.

Mchezo huo ulifikia hatua ya penalti baada ya timu hizo kufungana mabao 4-4 kwenye msako wa bingwa mpya kwenye ligi hiyo ambayo inadhaminiwa na Global Radio na Global TV Online.

Mabingwa hao walikabidhiwa kombe lao pamoja na medali kwenye mchezo huo huku Mburahati wao wakiambulia medali tupu pamoja na tuzo binafsi ambazo zilitolewa kwenye fainali hiyo.

Miongoni mwa tuzo iliyotolewa ni pamoja na ile ya kipa bora ambayo imechukuliwa na Adam Oseja wa Mburahati FC,mchezaji bora wa mchezo wa fainali akiwa ni Abdilah Mohamed wa Ilala FC.

Pia mfungaji bora kwenye ligi hiyo ni Ibrahim Ibadi wa Kijitonyama Sand Heroes ambaye alifunga jumla ya mabao 52,kocha bora ni Maliki Chanzi wa Ilala FC.