INAELEZWA kwamba, Klabu ya Yanga, imembakisha jijini Dar winga Simon Msuva baada ya kumpa ofa ya kujiunga na timu hiyo kwa mkataba wa mwaka mmoja.
Msuva ambaye aliitumikia Yanga kuanzia mwaka 2012 hadi 2017 alipoondoka kwenda Morocco kuichezea Difaâ El Jadida, kwa sasa yupo hapa nchini kutokana na kuwa na mgogoro na timu yake ya Wydad Casablanca ya nchini humo.
Kwa muda mrefu, Msuva amekuwa akihusishwa kutakiwa na Yanga, huku mwenyewe akisema malengo yake ni kwenda kucheza soka nje ya Tanzania.
Chanzo chetu kutoka Yanga, kimeliambia Spoti Xtra kwamba, klabu hiyo imemuwekea Msuva ofa ya shilingi milioni 150 ili asaini mkataba wa mwaka mmoja.
Mtoa taarifa huyo aliongeza kwamba, katika ofa hiyo, kwa mwezi mshahara atakuwa akilipwa zaidi ya shilingi milioni nane.
“Uongozi ulikaa mezani na Msuva na kumtaka arejee kucheza hapa nyumbani, lakini mwenyewe akasema amepata ofa kwa timu moja kutoka Argentina iliyomuwekea ofa ya mshahara wa dola 1800 kwa mwezi.
“Yanga wamemwambia aachane na timu hiyo, atapewa mara mbili ya mshahara huo ili asaini mkataba wa mwaka mmoja kwa thamani ya shilingi milioni 150.
“Pamoja na ushawishi huo, Msuva bado ameonekana kuhitaji zaidi kucheza nje, japo amewaahidi Yanga endapo atafanikiwa kupata kibali kutoka Wydad, anaweza kurudi mezani kujadili ofa hiyo. Katika kumshawishi zaidi, amepewa shilingi milioni 10 ambazo zipo nje ya mkataba,” kilisema chanzo hicho.
Hivi karibuni, Msuva alisema: “Suala la mimi kuzungumza na timu wala lisiwape shida, naweza kuzungumza na timu yoyote, lakini wapi nitacheza msimu ujao, nitawaambia.”