WAMILIKI CHELSEA WAANZA KUZINGUA MASHABIKI

WAMILIKI wapya wa Chelsea wakiongozwa na bilionea Todd Boehly, wameifumua bodi ya timu hiyo wakifukuza kazi vichwa kibao akiwemo gwiji Petr Cech, na hali hiyo imewafanya mashabiki kuwa na wasiwasi na kuonyesha hisia zao kwenye mitandao ya kijamii.

Cech ambaye ni kipa wa zamani wa Chelsea alikuwa mshauri wa ufundi na viwango klabuni hapo tangu 2019 na anamfuata mkurugenzi wa michezo Marina Granovskaia na mwenyekiti wa klabu hiyo, Bruce Buck kung’oka.

Lakini mashabiki wa Chelsea wamebaki wakiwa na wasiwasi juu ya hatima ya klabu hiyo na walivamia kwenye Twitter kuonyesha hofu yao.

Mmoja aliandika: “Sasa nina wasiwasi mkubwa kuhusu hawa wawiliki wapya. Wanavunja mfumo uliokuwepo na wanawafukuza wale wanaoijua klabu nje ndani. #ombaKwaAjiliYaChelsea.”

Mwingine aliandika: “Kuna mabadiliko makubwa kupita kiasi. Hakika ni kitu kibaya. Tuchel alipenda kufanya kazi naye. Alisema mara nyingi.”

Shabiki mwingine aliyeonekana kuwa na hasira, aliandika: “Tumekwisha. Hawa Wamarekani wataiua klabu yetu pendwa.”

Lakini mchambuzi wa Daily Mail, Martin Samuel, amesema mashabiki hawapaswi kumlaumu mmiliki, kwa kuwa ilikuwa ni lazima kufagia utawala wote wa Roman Abramovich.