YANGA WASHITUKA, YAFUATA BEKI GHANA

MABOSI wa Yanga wameiangalia ripoti ya Kocha Mkuu wa Yanga, Mtunisia Nasreddine Nabi haraka wakachukua maamuzi magumu ya kumfuata beki Mghana, Mohammed Alhassani.

Beki huyo anayemudu kucheza namba 4 na 5 anakipiga Klabu ya Heart of Oak inayoshiriki Ligi Kuu ya Ghana ambaye anakuja kuimarisha safu ya ulinzi.

Nabi hivi karibuni alisitisha mpango wa kusajili beki wa wa kigeni baada ya kuvutiwa na kiwango bora ambacho kimeonyeshwa na Ibrahim Hamad ‘Bacca’ wakati timu hiyo, ilipocheza mchezo wa ligi dhidi ya Tanzania Prisons.

Mmoja wa mabosi wa Yanga, ameliambia Championi Jumamosi kuwa licha ya ubora wa safu ya ulinzi, lakini uongozi umechukua maamuzi ya kumfuata beki huyo kwa ajili ya kuongezea nguvu kuelekea michuano ya kimataifa Afrika.

Bosi huyo alisema kuwa kikubwa wanataka kwenda katika michuano hiyo kikosi chao kikiwa kimekamilika katika kila sehemu kuanzia safu ya ulinzi, kiungo na ushambuliaji.

Aliongeza kuwa wanafurahia kusikia Caf kuongeza idadi ya wachezaji wa kuwasajili katika michuano ya kimataifa kutoka 30 hadi 40, licha ya kutotangazwa rasmi na shirikisho hilo la soka.

“Tunaheshimu uwezo na viwango vya mabeki wetu Mwamnyeto (Bakari), Job (Dickson), Bacca (Ibrahim Hamad) ambao wameonyesha kiwango bora katika ligi msimu huu.

“Mabeki hao ni tofauti na Bangala (Yannick) ambaye yeye ni kiraka na uongozi ungetamani kumuona mchezaji huyo angecheza namba sita na siyo beki wa nyuma kwa lengo la kupeleka mashambulizi goli la wapinzani.

“Hivyo haraka uongozi umeangalia kikosi, na kuchukua maamuzi ya kumfuata beki huyo Mghana kwa ajili ya mazungumzo ambayo kama yakienda vizuri basi tutamsajili,” alisema bosi huyo.

Msemaji wa Yanga, Haji Manara hivi karibuni alizungumzia usajili kwa kusema: “Yanga tumepanga kusajili wachezaji wanne pekee wa kigeni, lakini kama ikitokea kikosi kitahitajika maboresho, basi tutamuongeza mmoja.”