UCHAMBUZI WA GEORGE MPOLE, HAKUNA UBISHI NDO MFUNGAJI BORA MZAWA KWA SASA

NA Hussein Msoleka

MAISHA ya soka yana siri kubwa na changamoto nyingi, kuna wakati unaweza kutamani siku zirudi nyuma ili uweze kuona yale ambayo tuliyashuhudia huko nyuma.

Hivi sasa hakuna ubishi wowote kuwa George Mpole ndiye mshambuliaji bora zaidi mzawa kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu. Tayari straika huyu wa Geita Gold FC amehusika kwenye mabao 19 ya timu yake akifunga mabao 16 na ametoa pasi tatu za mabao.

Vita yake na Fiston Mayele kwenye mbio za ufungaji bora kwa kiasi kikubwa imeongeza mvuto kwenye ligi.

Kwa kipindi kirefu tulizoea kwenye mbio za kuwania kiatu cha dhahabu lazima utawakuta mastaa kutoka Simba, Yanga na Azam kwani ndiyo timu pekee ambazo hupewa kipaumbele cha kwanza kwenye kufanya vizuri kila msimu mpya wa ligi unapoanza lakini hali imekuwa tofauti msimu huu vita kubwa ipo kati ya Mayele wa Yanga na Mpole wa Geita Gold FC.

Kufanya vibaya kwa mastraika wa Simba John Bocco, Chris Mugalu na Meddie Kagere ambao wameshindwa kufikia rekodi zao za msimu uliopita kwa kufunga mabao zaidi ya 10.

Bocco ambaye alifunga mabao 16 msimu uliopita amefunga mabao matatu pekee, Kagere amefunga mabao saba huku Mugalu akiwa hajafunga bao lolote.

Msimu wa 2017/18 kwenye kikosi cha Mwadui FC ambayo hivi sasa ipo Ligi Daraja la Pili (First League) kulikuwa na straika aliyeitwa Salim Aiyee.

Aiyee alikuwa na msimu bora sana kwenye Ligi Kuu Bara akimaliza na mabao zadi ya 15 kwenye ligi jambo ambalo lilifanya aimbwe kwenye kila kona ya vijiwe vya kidigitali.

Aiyee alitabiriwa kuwa miongoni mwa mastraika ambao watakuwa tishio kwenye ligi katika siku za usoni lakini msimu uliofuata alijikuta kwenye wakati mgumu ndani ya kikosi cha KMC ambapo alimaliza msimu akiwa na bao moja kwenye ligi.

Si Aiyee pekee wapo nyota wengi ambao walifanikiwa kufanya makubwa wakiwa kwenye vikosi vyao na walipojiunga na timu nyingine mambo yaliwaendea kombo. Wachezaji kama Mohammed Rashid, Marcel Kaheza, Adam Salamba ni mfano wa wachezaji wachache ambao walifanya makubwa na baada ya hapo wamepotelea kusikojulikana.

Tayari kuna tetesi kuwa Simba na Azam FC zinaiwinda saini ya Mpole kwa ukaribu zaidi hivyo chaguo ni lake kusuka au kunyoa aidha asalie Geita Gold au aende kutafuta changamoto mpya ambayo iliwashinda nyota wengi huko nyuma.

Salamba ni miongoni mwa wachezaji ambao waliziingiza Simba na Yanga kwenye vita kubwa ya kuiwinda saini yake kutokana na ubora ambao aliuonyesha akiwa na kikosi cha Lipuli chini ya kocha Seleman Matola na Simba walifanikiwa kuinasa saini yake lakini straika huyu hakufikia kile ambacho uongozi na mashabiki wengi wa Simba walikitarajia kutoka kwake.

Moto ambao yupo nao Mpole kwenye ligi msimu huu ni wazi kuwa hakuna timu ambayo haitamani kuwa na mchezaji wa aina yake kikosini uwezo wake wa kutumia miguu yote miwili kwa ufasaha, anafunga mabao ya aina zote nje na ndani ya boksi shida inakuja je ataendeleza hapo alipoishia msimu ujao?

Au ndiyo ataingia kwenye anga za akina Aiyee, Salamba na Mo Rashid baada ya kufanya vizuri kwenye msimu mmoja na msimu uliofuata hawakuonyesha maajabu yoyote na wamepotelea kusikojulikana wakiishia kuonyeshwa mlango wa kutokea kwenye timu zao.

Mpole ana kazi kubwa ya kutengeneza njia yake ambayo itafanya tumpate mrithi sahihi wa Bocco kwenye Ligi Kuu Bara pamoja na timu ya taifa endapo atafanikiwa kujiunga na timu kubwa za Mzizima, hatakiwi kubweteka bali kuendeleza pale alipoishia ili aweze kujitengenezea njia yake kuelekea kilele cha mafanikio.

Tunatamani kuwa na wachezaji wazawa ambao watakuwa na mchango mkubwa kwenye klabu zao ili tuweze kuwa na timu ya taifa imara hivyo George Mpole anatakiwa kutambua kuwa ana deni kubwa kwa wapenzi wa soka nchini ambao ni wazi wengi wao wanatamani kumuona akiwa mfungaji bora msimu huu.