SIMBA mpya mbona mtapigwa sana! Hiyo ni baada ya Simba kuweka wazi kuwa watafanya usajili ambao utawafanya msimu ujao kufanya vyema mara baada ya msimu huu kuwa mbaya kwao.
Rais wa Heshima, Mohamed Dewji ‘Mo’, ameshashauri kuwa timu hiyo inatakiwa ifumuliwe, na yupo tayari kumwaga pesa za usajili.
Tayari Simba imeshamnasa mshambuliaji hatari, Moses Phiri kutoka Zanaco ya Zambia na anakwenda kuungana na Mzambia mwenzake, fundi Clatous Chama kutengeneza safu ya kutisha ya ushambuliaji pale mbele. Wengine wanafuata.
Mtendaji Mkuu wa Simba (CEO), Barbara Gonzalez, mapema wiki hii wakati akizindua mradi wa ujenzi wa uwanja wa mazoezi wa timu hiyo uliopo Bunju, alisema kuwa: “Katika kuhakikisha kuwa Simba inarejea katika ubora wake, lazima tutafanya usajili wa maana ili tuweze kubeba makombe yote msimu ujao ambayo msimu huu tumeyakosa.”
Simba katika usajili tayari wameshamtambulisha Phiri kutoka katika Klabu ya Zanaco ambaye staa huyo hucheza katika maeneo yote ya mbele kuanzia wingi zote mbili za kulia na kushoto lakini kama namba kumi na mshambuliaji wa mwisho namba tisa.
Ukiachana na usajili wa mshambuliaji huyo, tayari Gazeti la Championi Jumatatu, limebaini Simba kukamilisha usajili wa wachezaji kama Victor Akpan ambaye anatokea katika Klabu ya Coastal Union huyu yeye akiwa na uwezo wa kucheza kama kiungo mkabaji.
Katika eneo la ulinzi ukiachana na Akpan ambaye ni kiungo mkabaji, Simba ipo katika hatua za mwisho kumalizana na beki wa kimataifa wa timu ya taifa ya Burundi, Frederick Nsabiyumva.
Ukiachana na huyo Simba pia imekamilisha usajili wa winga wa pembeni Augstine Okra kutoka katika Klabu ya Bechem ya nchini Ghana ambaye winga huyu ni moto wa kuotea mbali akifananishwa na Luis Miquissone ambaye aliwahi kuwika ndani ya Simba.
Kwa upande wa ushambuliaji wa kati Simba pia inatajwa kumalizana na mshambuliaji hatari Cesar Lobi Manzoki kutoka katika Klabu ya Vipers ya nchini Uganda.
Manzoki msimu huu amefunga mabao 19 ndani ya ligi hiyo na kuwa mfungaji bora wa ligi hiyo jambo ambalo ni faida kwa Simba kusajili mshambuliaji hatari kama huyo ambaye ni wazi atakuja kumaliza changamoto ya Simba ya ukame wa mabao.
Hivyo kama usajili huo utatiki basi kikosi cha Simba kinaweza kupangwa hivi na watu wakala bao za kutosha:
Aishi Manula 2. Shomari Kapombe 3. Mohammed Hussein 4. Frederic Nsabiyumva 5. Inonga Baka 6. Victor Akpan 7. Augustine Okra 8. Sadio Kanoute 9. Cezar Manzoki 10. Moses Phiri 11. Clatous Chama