KOCHA HUYU ATAJWA KUBEBA MIKOBA YA PABLO

IMEELEZWA kuwa jina la Josef Vukusic ambaye amewahi kuinoa Klabu ya Polokwane na Amazulu za Afrika Kusini ambaye aliletwa duniani Agosti 3,1964 akiwa na miaka 57 anatajwa kuwa miongoni mwa makocha watakaorithi mikoba ya Pablo Franco ndani ya Simba.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya Simba zimeeleza kuwa kwa sasa mchakato huo umefika hatua nzuri kwa kufanya mchujo wa majina ya makocha ambao wameomba kazi ya kukifundisha kikosi hicho.

“Kuna orodha ya makocha wengi ambao wameomba kuifundisha Simba hasa ukizingatia kwamba Simba ni moja ya timu ambazo zinafanya vizuri ndani ya ligi na nje kimataifa hivyo inajulikana,” ilieleza taarifa hiyo.

Ahmed Ally, Mkuu wa Idara ya Habari Simba amesema kuwa watamtangaza kocha mpya mapema kabla ya ligi kuisha na atakuja kufanya usajili pamoja na kuanza maandalizi ya msimu mpya.

“Ipo wazi kwamba kuna majina mengi ya makocha ambao wameomba kuifundisha Simba lakini kwa sasa ambacho kinafanyika ni mchujo ili kuweza kujua nani atakuja mapema kabla ya maandalizi ya msimu mpya kuanza,” amesema.

Kwa sasa timu hiyo ipo chini ya Selaman Matola ambaye amekiongoza kikosi hicho kwenye mechi mbili ilikuwa mbele ya Mbeya City na KMC na zote alisepa na pointi tatu kwenye kila mechi.