KIPA WA ZAMANI AMUONDOA KAKOLANYA SIMBA

KOCHA wa Makipa na nyota wa zamani wa Sigara, Mtibwa Sugar na Yanga, Peter Manyika amewaangalia makipa wa sasa wa Simba, kisha kumchomoa Beno Kakolanya katika kikosi hicho, ili atafute maisha mengine kama anahitaji kulinda kiwango chake.

Ubora wa Kakolanya ulionekana katika mchezo wa Simba dhidi ya Yanga akiwa katika lango la Wanajangani na aliweza kupangua mashambulizi yaliyopigwa na nyota wa Simba na kushawishika kusajiliwa akiwa chini ya Aishi Manula.

Akizungumza na Mwanaspoti, Manyika alisema Kakolanya ni kipa mzuri, lakini ubora wake utaisha endapo akishindwa kuuonyesha kwa kupata mechi nyingi za kucheza.

“Kusema ukweli Kakolanya ni bora kama anataka mafanikio ndani ya mchezo akatafute maisha mengine, kama mafanikio hayako ndani ya mchezo aendelee kuwepo Simba, lakini kama sio hivyo ajiongeze kulinda ubora wake,” alisema Manyika na kuongeza;

“Shida sio timu wala nini shida ni yeye mwenyewe mchezaji, na sio mchezaji anatoka kwenye timu kwa sababu ya kutokuwa na kiwango hapana, ni kwa kuwa anahitaji kupata nafasi ya kucheza ndani ya kikosi ili akilinde kipaji chake.”

Alisema kwa namna ambavyo hapati namba katika kikosi hicho hawezi kukua atajikuta anasalia alipo ni nyota mzuri ila ajitahidi kujiongeza.
Advertisement

Manyika alisema kila timu kuna chaguo la kocha kama timu kubwa kunakuwepo na tofauti katika michezo wanayocheza, lakini wapatapo nafasi ya kucheza kujiamini asilimia 100 kunakosekana.

Kakolanya alitua Simba akitokea timu ya Yanga.