BEKI SIMBA AGOMEA MKATABA, AOMBA KUSEPA

 INATAJWA kuwa beki wa kati wa Simba, Ibrahim Ame anayecheza kwa mkopo Mtibwa amegoma kuongeza mkataba kwa mabosi wake hao huku ikielezwa kuwa kuna mpango wa kujiunga na Coastal Union.

Ame alijiunga na Simba msimu wa 2020/21 akitokea Coastal Union na kusaini mkataba wa miaka miwili ambao unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu.

Mmoja wa watu wa karibu na mchezaji huyo ameliambia Championi Jumamosi, kuwa pamoja na Simba kumlipa Ame mishahara yote alipokuwa Mtibwa, lakini amegoma kurejea kikosini hapo na kwamba ameomba arudi Coastal ili aweze kupata nafasi kubwa ya kucheza.

“Naomba nikuambie tu kuwa Ame amegoma kusaini tena Simba na tulipofuatilia tumegundua kuwa, zoezi la kuboresha kikosi linawafanya wachezaji wengi waliowahi kuitumikia kuogopa tena kurudi kwa hofu ya namba.

“Kwa maana kila mmoja anaamini maboresho ya msimu huu yatawafanya kurudi na kukaa benchi tena.”

Championi lilizungumza na Msemaji wa Coastal Union, Jonathan Tito ambapo alisema: “Ni kweli Ame ameomba kurejea mwishoni mwa msimu, japo aliondoka kwa mbwembwe na jeuri, ila sisi tumemuonyesha uungwana na kwamba msimu ujao tutakuwa naye tena.”