SIMBA SC ipo katika mazungumzo ya mwisho ya kukamilisha usajili wa mshambuliaji Augustine Okrah anayeichezea Bechem United FC ya Ghana.
Timu hiyo imepanga kukiboresha kikosi chao kitakachowavusha hatua ya robo fainali ya michuano ya kimataifa watakayoshiriki msimu ujao baada ya misimu ya karibuni kuishia hatua hiyo.
Wakati mshambuliaji huyo akitarajiwa kutua, Simba imepanga kuachana na washambuliaji wa kimataifa Mnyarwanda, Meddie Kagere na Chris Mugalu raia wa DR Congo.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Spoti Xtra, Simba ipo katika mazungumzo mazuri na uongozi wa mshambuliaji huyo.
Mtoa taarifa huyo alisema mazungumzo hayo ni katika kukubaliana mambo mengi ikiwemo kusaini mkataba wa miaka miwili wenye kipengele cha kuongeza baada ya kumalizika wa awali.
Aliongeza kuwa, mshambuliaji huyo anasajiliwa baada ya Simba kumkosa Victorien Adebayor raia wa Niger ambaye muda wowote atatambulishwa RS Berkane ya Morocco.
“Tumepanga kufanya usajili wetu kimyakimya, hiyo ndio sababu ya kutotusikia sana taarifa zetu za usajili, tayari wapo wachezaji tuliokuwa katika hatua za mwisho kukamilisha usajili wao.
“Ukimya huu wa usajili wetu umetokana na baadhi ya klabu kubwa kama Wydad Casabalanca, RS Berkane, Al Ahly, Kaizer Chiefs kuingilia kila usajili tuliopanga kuufanya.
“Kati ya wachezaji tuliokuwa nao katika hatua za mwisho za kukamilisha usajili wake ni Augustine Okrah anayecheza nafasi ya ushambuliaji ambaye atakuja kuchukua nafasi ya Mugalu na Kagere,” alisema mtoa taarifa huyo.
Akizungumzia usajili, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ alisema: “Usajili wetu tumepanga kuwa wa kimyakimya, hatutaki kufanya kama wengine wanavyofanya.”
Mshambuliaji huyo mwenye miaka 28, msimu huu amefanikiwa kufunga mabao 14 katika michezo 31 aliyocheza.