IMEELEZWA kuwa Simba imefikia makubaliano mazuri na uongozi wa Coastal Union ya kumnunua kiungo mkabaji Mnigeria, Victor Akpan.
Kiungo huyo ni kati ya viungo bora wakabaji walioonyesha kiwango bora katika msimu huu ambaye anakuja Simba kuchukua nafasi ya Thadeo Lwanga ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu.
Mnigeria huyo ndio alikuwa kikwazo katika michezo miwili ya Ligi Kuu Bara walipokutana na Simba huku akifanikiwa kumfunga bao la kiufundi kipa wa timu hiyo, Aishi Manula umbali wa mita 20.
Kwa mujibu wa taarifa imeelezwa kuwa Simba walitarajiwa kukutana na viongozi wa Coastal kwenye moja ya hoteli kubwa jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kukamilisha dili hilo la usajili.
Mtoa taarifa huyo alisema kuwa kabla ya kikao hicho kufanyika, tayari yapo baadhi ya makubaliano waliyofikia kati ya Simba na Coastal ambao wamekubali kumpa baadhi ya mahitaji yenye maslahi ikiwemo kumpatia dau nono la usajili.
Aliongeza kuwa pia Simba wamekubali kumpatia mshahara mzuri, gari ya kutembelea na nyumba atakayokaa kwa kipindi chote cha miaka miwili atakachokuwepo Simba.
“Akpan atakuwa mchezaji wa pili kusajiliwa kutoka Coastal ni baada ya kumalizana na kiungo mshambuliaji Sopu (Abdul Selemani) ambaye yeye ni mchezaji huru ambaye anajiunga na Simba bure.
“Tayari uongozi wetu wa Simba tumefikia makubaliano mazuri na Coastal kwa ajili ya kufanikisha dili hilo la usajili na leo (jana) usiku tunatarajia kukutana na viongozi wa Coastal kwa ajili ya kukamilisha dili hilo.
“Hiyo itakuwa hatua ya mwisho, kwani tayari tulishamalizana nao na kilichobakia ni kukutana na mchezaji mwenyewe kabla ya kumpa mkataba huo wa miaka miwili Simba.
“Tumekamilisha dili hilo mapema, ni baada ya kupata taarifa za baadhi ya timu kuonyesha nia ya kumhitaji ikiwemo Azam FC,” alisema mtoa taarifa huyo.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alipotafutwa kuweka mizania alisema: “Muda wa usajili bado na kingine tunamsubiria kocha mpya tutakayemtangaza wiki mbili hizi ambaye atakuja kusimamia usajili huo, hivyo tusubirie muda ufikie tutaweka wazi.”