MAJINA ya nyota wawili wanaocheza ndani ya kikosi cha Yanga kinachonolewa na Kocha Mkuu, Nasreddine nabi leo Juni 14,2022 yametajwa bungeni.
Ni Fiston Mayele mshambuliaji namba moja ndani ya Yanga akiwa ametupia mabao 14 na pasi tatu pamoja na Feisal Salum ambaye alitupia bao la ushindi kwenye mchezo wa nusu fainali Kombe la Shirikisho uliochezwa Uwanja wa CCM Kirumba dhidi ya Simba.
Mastaa hao wametajwa na Waziri wa Fedha na Mipango,Dk Mwigulu Nchemba bungeni, Dodoma wakati Mwigulu akiwasilisha mapendekezo ya Serikali kuhusu makadirio ya Mapato na matumizi 2022-2023.
Mara baada ya Mwigulu kutaja majina ya wachezaji hao wabunge walianza kushangilia kwa kupiga makofi jambo lililoleta furaha kwa wabunge wengi ambao ni mashabiki wa Yanga.
“Nampongeza GSM kwa kurejesha furaha ya wananchi hasahasa kwa usajili wa Fiston Mayele. Mayele amekuwa maarufu.
Waziri Mwigulu pia ameipongeza Klabu ya Simba kwa kufanya vizuri katika mashindano ya Kimataifa.
“Nawapongeza sana na marafiki zangu Klabu ya Simba kwa kuwakilisha vyema kwenye mashindano ya kimataifa, wananijua mara zote kimataifa tuko pamoja, siwezi kukana Bendera ya Taifa langu kwa ajili ya utani wa jadi,”amesema.
Kwenye mashindano ya Kimataifa Simba iliishia hatua ya robo fainali baada ya kuondolewa na Orlando Pirates ugenini kwa mikwaju ya penalti.