KOCHA KAIZER CHIEFS AMALIZANA NA SIMBA

BAADA ya kufanya mazungumzo mazito na mabosi wa Simba SC, inaelezwa kwamba kocha wa zamani wa Kaizer Chiefs, Stuart Baxter, wamefikia makubaliano mazuri, lakini ameomba kwanza kurejea kwao Uingereza.

Kocha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Afrika Kusini na England U19, juzi alifanya mazungumzo na mabosi wa Simba kwa ajili ya kukamilisha dili la kuifundisha timu hiyo.

Simba kwa sasa inasaka kocha wa kuchukua mikoba ya Pablo Franco ambaye ametimuliwa kikosini hapo Mei 30, mwaka huu.

Baxter amefanya mazungumzo na Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez akiwa na Mshauri wa Rais wa Heshima wa Simba, Crescentius Magori na Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi, Mulamu Ng’ambi katika kikao kilichofanyika Afrika Kusini.

Taarifa kutoka kwa vyanzo vya kuaminika vilivyopo Afrika Kusini, zinaeleza kwamba mazungumzo ya kocha huyo na mabosi wa Simba yameenda vizuri na jana usiku alirejea zake Uingereza kwa ajili ya mipango ya kujiandaa kwa kazi mpya.

“Kocha tayari ameshaondoka hapa Afrika Kusini na mazungumzo yake na mabosi wa Simba kwa asilimia 90 yamekwenda vizuri.

“Sehemu kubwa ya mazungumzo yao yamesimama pazuri na huenda Baxter akawa ndiye kocha mpya wa Simba, lakini inatazamiwa na yeye atakavyorejea kutoka Uingereza ambapo amekwenda kuweka mambo yake sawa ikiwemo ishu za kifamilia,” alisema mtoa taarifa huyo.