UONGOZI wa Azam FC umeweka wazi kuwa kwa sasa hesabu zao ni kwa msimu ujao kurejea kwa kasi na nguvu zaidi.
Hizi zinakuwa ni hesabu mpya za Azam FC inayotumia Uwanja wa Azam Complex kwa mechi zao za nyumbani.
Tayari matumaini ya kutwaa mataji ndani ya Azam FC yameyeyuka kwa kuwa wamefungashiwa virago kwenye Kombe la Shirikisho hatua ya nusu fainali na kwenye ligi wapo nafasi ya 4 na pointi 37.
Ofisa Habari wa Azam FC, Zakaria Thabit amesema kuwa matokeo ambayo wameyapata msimu huu hayajawafurahisha hivyo watafanya vizuri wakati ujao.
“Ipo wazi kwamba matokeo ambayo tumeyapata msimu huu hayajatufurahisha kwa kuwa tuna wachezaji wazuri na wao wanapenda kuona matokeo mazuri lakini hayajapatikana.
“Ambacho kwa sasa tunakifanya ni kuweza kuona tunamaliza msimu kwenye nafasi nzuri itakayotupa uwezo wa kushiriki mashindano ya kimataifa,tutajipanga huko ili tufanye vizuri zaidi kwa msimu ujao,” amesema Thabit.