KOCHA STARS AFICHUA TANZANIA ITAKAVYOFUZU AFCON

BAADA ya kupoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya timu ya Taifa ya Algeria katika mchezo wa kusaka tiketi ya kufuzu Kombe la mataifa ya Afrika (Afcon 2023), Kocha Mkuu wa Stars, Kim Poulsen ameweka wazi kuwa atatumia michezo miwili ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (Chan), kama sehemu ya kujiaandaa na michezo ya kufuzu Afcon.

Juzi Jumatano Stars wakiwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, walikubali kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Algeria katika mchezo wa pili wa kusaka tiketi ya kufuzu Afcon.

Kufuatia kipigo hicho Tanzania sasa inakamatia nafasi ya tatu katika msimamo wa Kundi F la michuano hiyo, ambapo Algeria wanaongoza msimamo na pointi zao sita ambapo timu zote zimecheza mechi mbili. Niger ni wa pili wakiwa na pointi mbili, na Uganda ni ya mwisho ikiwa na pointi moja kama ilivyo kwa Stars.

Akizungumza na Championi Ijumaa, Kocha Kim alisema: “Matokeo yetu dhidi ya Algeria hatukuyatarajia, lakini tunapaswa kukubali kuwa tulicheza dhidi ya timu bora Afrika ambayo tunapaswa kujifunza vingi kutoka kwao.

“Bado tuna nafasi ya kufuzu Afcon, jambo zuri kwetu ni kuwa tutakuwa na michezo ya michuano ya Chan dhidi ya Somalia kabla ya kucheza tena hizi mechi za kufuzu Afcon.

“Kwa kuwa sehemu kubwa ya wachezaji wangu wanacheza ligi ya ndani, basi mpango wetu ni kutumia michezo hiyo miwili kujiandaa na michezo dhidi ya Uganda ambayo tunapaswa kushinda ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu.”