MENEJA wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema nyota wawili waliokuwa majeruhi katika kikosi chao, Aishi Manula na Shomari Kapombe, wameanza mazoezi rasmi kujiandaa kuikabili Yanga SC kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa, Jumamosi hii.
Manula alipata maumivu ya mkono muda mfupi kabla ya mchezo wa ligi kati ya Geita Gold v Simba na Kapombe yeye alipata maumivu muda wa mchezo.
Ally amesema wachezaji wanaendelea na maandalizi kuelekea mchezo huo huku wakiutumia Uwanja wa Gwambina kwa ajili ya mchezo huo.
“Tunaendelea na maandalizi yetu ambapo kwa sasa tunautumia Uwanja wa Gwambina kufanya mazoezi, kiukweli maandalizi yanaendelea vizuri na mkakati wetu ni kuhakiisha tunapata ushindi mbele ya Yanga.
“Habari njema ni kwamba wachezaji wetu wawili ambao ni Shomari Kapombe aliyeumia nyama za paja tulipocheza dhidi ya Geita pamoja na Aishi Manula ambaye alikatwa na vioo kwenye vidole, wanaendelea vizuri na tayari wameanza mazoezi na wenzao, tunaamini kuelekea mchezo ujao watakuwa sehemu ya kikosi kitakachopambana na Yanga.