MABOSI WA SIMBA WAONGOZWA NA MO KUIJADILI YANGA

KUELEKEA mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports kati ya Yanga dhidi ya Simba, Rais wa Heshima wa Klabu ya Simba, Mohamed Dewji ‘Mo Dewji’, ameitisha kikao cha ghafla ili kuona wanajipangaje kuwamaliza wapinzani wao hao.

Jumamosi hii, Simba itakuwa na kibarua kizito mbele ya Yanga, katika mchezo huo utakaochezwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Habari zimeeleza kuwa, kutokana na uzito wa mchezo huo, Mo Dewji amewataka Mtendaji Mkuu, Barbara Gonzalez, Mwenyekiti wa Klabu, Murtaza Mangungu na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Salim Abdallah ‘Try Again’, kukutana ili kujipanga kuona wanaimaliza vipi Yanga.

“Tunamshukuru Mungu kwa kuwaonesha viongozi wetu umuhimu wa mchezo ujao dhidi ya Yanga, ambapo sifa zote ziende kwa Mo Dewji, ambaye ameomba wakutane haraka ili kuona namna ya kushinda mchezo huo.

“Mo Dewji alikuwa Marekani kwenye shughuli zake, ila amepata muda wa kuwasiliana na Mwenyekiti wa Bodi, Try Again aliyekuwa Dubai na kumtaka wakutane haraka kwa ajili ya kuhakikisha tunaweka mipango madhubuti ya kutetea kombe letu la FA, maana tayari ubingwa wa ligi tumeuweka rehani kwa Yanga.

“Kikao hicho kilitakiwa kufanyika mapema na kwamba tayari Try Again ameshawasili nchini kutoka Dubai, hivyo alitakiwa kuwasiliana na Barbara ambaye yupo Mwanza pamoja na Mangungu ili waone wapi pa kufanyia, huku Mo Dewji akishiriki kwa njia ya mtandao,” kilisema chanzo hicho.

Chanzo Spoti Xtra.